2 Wafalme 8:16-29, 2 Wafalme 9:1-37 NEN

2 Wafalme 8:16-29

Yehoramu Mfalme Wa Yuda

(2 Nyakati 21:1-20)

8:16 2Fal 1:17; 2Nya 21:1-4Katika mwaka wa tano wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, wakati huo Yehoshafati akiwa mfalme wa Yuda, Yehoramu mwana wa Yehoshafati akaanza kutawala kama mfalme wa Yuda. Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka minane. Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alimwoa binti wa Ahabu. Akatenda maovu machoni pa Bwana. 8:19 2Sam 21:17Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi mtumishi wake, Bwana hakutaka kuiangamiza Yuda. Alikuwa ameahidi kuidumisha taa kwa ajili ya Daudi na wazao wake milele.

8:20 1Fal 22:47Wakati wa Yehoramu, Edomu waliasi dhidi ya Yuda na kujiwekea mfalme wao wenyewe. Basi Yehoramu akaenda Sairi pamoja na magari yake yote ya vita. Waedomu wakamzunguka yeye na majemadari wake wa magari yake ya vita, lakini akaondoka, akapenya usiku na kuwashambulia Waedomu. Hata hivyo, jeshi lake likatorokea nyumbani mwao. 8:22 Mwa 27:40; Yos 21:13Hadi leo Edomu wameasi dhidi ya Yuda. Libna pia wakaasi wakati huo huo.

Kwa matukio mengine ya utawala wa Yehoramu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Yehoramu akalala pamoja na baba zake, na akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.

Ahazia Mfalme Wa Yuda

(2 Nyakati 22:1-6)

8:25 2Fal 9:29Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alianza kutawala. 8:26 2Fal 8:18; 1Fal 16:23Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri mfalme wa Israeli. 8:27 1Fal 16:30; 15:26Akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, na kutenda maovu machoni pa Bwana, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alikuwa ameoa kutoka nyumba ya Ahabu.

8:28 Kum 4:43; 2Fal 9:1, 14Ahazia akaenda vitani na Yoramu mwana wa Ahabu kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu. 8:29 1Fal 21:29; 2Fal 10:13Hivyo Mfalme Yoramu akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa na Waaramu huko Ramothi8:29 Yaani Rama kwa Kiebrania. alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu.

Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.

Read More of 2 Wafalme 8

2 Wafalme 9:1-37

Yehu Atiwa Mafuta Kuwa Mfalme

9:1 1Sam 10:5; 2Fal 8:28Nabii Elisha akamwita mtu mmoja kutoka kwa wana wa manabii na kumwambia, “Jikaze viuno, uichukue hii chupa ya mafuta, na uende Ramoth-Gileadi. Ukifika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi. Enda kwake, umtenge na wenzake, na umpeleke katika chumba cha ndani. 9:3 1Fal 19:16Kisha chukua hii chupa na umimine mafuta juu ya kichwa chake, nawe utangaze, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ Kisha ufungue mlango na ukimbie; usikawie!”

Basi yule kijana nabii akaenda Ramoth-Gileadi. Wakati alipofika, akawakuta maafisa wa jeshi wameketi pamoja, akasema, “Nina ujumbe wako, ee jemadari.”

Yehu akauliza, “Kwa yupi miongoni mwetu?”

Akamjibu, “Kwako wewe, jemadari.”

9:6 1Fal 19:16Yehu akainuka na kuingia ndani ya nyumba. Ndipo yule nabii akamimina mafuta juu ya kichwa cha Yehu na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya watu wa Bwana, yaani Israeli. 9:7 Mwa 4:24; Kum 32:43Inakupasa uiangamize nyumba ya bwana wako Ahabu, nami nitalipiza kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii na damu ya watumishi wote wa Bwana iliyomwagwa na Yezebeli. 9:8 1Sam 25:22Nyumba yote ya Ahabu itaangamia. Nitamkatilia mbali kila mzaliwa wa kiume wa Ahabu katika Israeli, aliye mtumwa ama aliye huru. 9:9 1Fal 14:10Nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama ile nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama ile nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya. 9:10 1Fal 21:23Kuhusu Yezebeli, mbwa watamla kwenye kiwanja huko Yezreeli, wala hakuna mtu atakayemzika.’ ” Kisha akafungua mlango na kukimbia.

9:11 Yn 10:20; 1Sam 10:11Yehu alipotoka nje na kurudi kwenda kwa maafisa wenzake, mmoja wao akamuuliza, “Je, kila kitu ni salama? Kwa nini huyu mwenye wazimu alikuja kwako?”

Yehu akajibu, “Wewe unamfahamu huyo mtu, na aina ya mambo ambayo yeye husema.”

Wakasema, “Hiyo siyo kweli! Tuambie.”

Yehu akasema, “Haya ndiyo aliyoniambia: ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ ”

9:13 Mt 21:8; 2Sam 15:10Wakaharakisha kuvua mavazi yao, na kuyatandaza chini ya Yehu ili akanyage juu kwenye ngazi ya nje. Kisha wakapiga tarumbeta na kupaza sauti wakisema, “Yehu ni mfalme!”

Yehu Anamuua Yoramu Na Ahazia

9:14 Kum 4:43; 2Fal 8:28Basi Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akafanya shauri baya dhidi ya Yoramu. (Wakati huu, Yoramu na Israeli wote walikuwa wakiilinda Ramoth-Gileadi dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu, 9:15 2Fal 8:29lakini Mfalme Yoramu alikuwa amerudishwa Yezreeli ili kujiuguza kutokana na majeraha ambayo Waaramu walimtia katika vita na Hazaeli mfalme wa Aramu.) Yehu akasema, “Kama hii ndiyo nia yenu, msimruhusu hata mmoja kutoroka nje ya mji kwenda kupeleka habari huko Yezreeli.” 9:16 2Nya 22:7Ndipo Yehu akaingia katika gari lake la vita na kuendesha kwenda Yezreeli, kwa sababu Yoramu alikuwa amepumzika huko, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameenda kumwona.

9:17 1Sam 14:16Mlinzi aliyesimama juu ya kinara cha Yezreeli alipoona askari wa Yehu wanakuja, akaita akisema, “Naona askari wanakuja.”

Yoramu akaamuru, “Mtwae mpanda farasi umtume akakutane nao na kuuliza, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”

Mpanda farasi akaondoka kwenda kukutana na Yehu na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme: ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”

Yehu akamjibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”

Mlinzi akatoa habari, “Mjumbe amewafikia lakini harudi.”

Basi mfalme akamtuma mpanda farasi wa pili. Wakati alipowafikia akasema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”

Yehu akajibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”

9:20 2Sam 18:27Yule mlinzi akatoa taarifa akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini hata yeye harudi. Uendeshaji ule ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi, anaendesha kama mwenye wazimu!”

9:21 1Fal 21:1Yoramu akaagiza, akasema, “Weka tayari gari langu la vita.” Na baada ya gari kuwa tayari, Yoramu mfalme wa Israeli, na Ahazia mfalme wa Yuda, wakaondoka kila mmoja kwenye gari lake ili kukutana na Yehu. Walikutana naye katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. 9:22 1Fal 18:19Yoramu alipomwona Yehu akauliza, “Je, Yehu, umekuja kwa amani?”

Yehu akajibu, “Kunawezaje kuwa na amani wakati ibada za sanamu na uchawi wa mama yako Yezebeli ungaliko?”

9:23 2Fal 11:14Yoramu akageuka nyuma na kukimbia, akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini, Ahazia!”

9:24 1Fal 22:34Kisha Yehu akatwaa upinde wake na kumchoma Yoramu katikati ya mabega. Mshale ukapenya kwenye moyo wake, naye akaanguka ghafula ndani ya gari lake. 9:25 1Fal 21:19-22Yehu akamwambia Bidkari, mwendeshaji wa gari lake, “Mwinue na umtupe katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. Kumbuka jinsi mimi na wewe tulivyokuwa tukiendesha pamoja magari yetu nyuma ya Ahabu baba yake, wakati Bwana alipotoa unabii huu kumhusu: 9:26 1Fal 21:19‘Jana niliona damu ya Nabothi na damu ya wanawe, nami kwa hakika nitakufanya uilipe juu ya shamba hili, asema Bwana.’ Sasa basi, mwinue na umtupe juu ya kiwanja, kulingana na neno la Bwana.”

9:27 Amu 1:27; 2Fal 23:29Wakati Ahazia mfalme wa Yuda alipoona kilichotokea, akakimbia kupitia barabara ya Beth-Hagani. Yehu akamkimbiza akipaza sauti na kusema, “Muue naye pia!” Wakamjeruhi katika gari lake kwenye njia ielekeayo Guri karibu na Ibleamu, lakini akatorokea Megido na akafia huko. 9:28 2Fal 23:30Watumishi wake wakambeba kwa gari la vita na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika pamoja na baba zake kwenye kaburi lake katika Mji wa Daudi. 9:29 2Fal 8:25(Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala katika Yuda.)

Yezebeli Auawa

9:30 Yer 4:30; Eze 23:40Kisha Yehu akaenda Yezreeli. Yezebeli aliposikia habari hii, akayapaka macho yake rangi, akatengeneza nywele zake na kutazama nje dirishani. 9:31 1Fal 16:9-10Yehu alipokuwa akiingia langoni, Yezebeli akasema, “Je, umekuja kwa amani, Zimri, wewe muuaji wa bwana wako?”

Yehu akaangalia juu dirishani na kuita, “Je, ni nani aliye upande wangu? Ni nani?” Matowashi wawili au watatu wakamtazama. 9:33 Za 7:5Yehu akasema, “Mtupeni huyo mwanamke chini!” Kwa hiyo wakamtupa chini, nayo baadhi ya damu yake ikatapanyika ukutani na nyingine juu ya farasi walipokuwa wakimkanyaga kwa miguu yao.

9:34 1Fal 16:31Yehu akaingia ndani, akala na akanywa. Akasema, “Mshughulikieni huyo mwanamke aliyelaaniwa. Mzikeni, kwa sababu alikuwa binti wa mfalme.” Lakini walipotoka kwenda kumzika, hawakukuta kitu chochote isipokuwa fuvu la kichwa, miguu yake na mikono. 9:36 Za 68:23; 1Fal 21:23Wakarudi na kumwambia Yehu, ambaye alisema, “Hili ndilo neno la Bwana alilosema kupitia kinywa cha mtumishi wake Eliya Mtishbi, kwamba: Katika kiwanja cha Yezreeli, mbwa wataikula nyama ya Yezebeli. 9:37 Za 83:10; Yer 8:2Maiti ya Yezebeli itakuwa kama mavi shambani katika uwanja wa Yezreeli, kwamba hakutakuwepo mtu atakayeweza kusema, ‘Huyu ndiye Yezebeli.’ ”

Read More of 2 Wafalme 9