2 Wafalme 4:38-44, 2 Wafalme 5:1-27, 2 Wafalme 6:1-23 NEN

2 Wafalme 4:38-44

Mauti Ndani Ya Chungu

4:38 2Fal 2:1; 8:1Elisha akarudi Gilgali, nako huko kulikuwa na njaa katika eneo lile. Wakati wana wa kundi la manabii walipokuwa wanakutana naye, akamwambia mtumishi wake, “Teleka chungu kikubwa jikoni uwapikie manabii.”

Mmoja wao akatoka kwenda mashambani kuchuma mboga na akapata mtango mwitu. Akachuma matango na kujaza nguo yake aliyoikunja ili kubebea. Aliporudi, akayakatakata na kuyatumbukiza ndani ya chungu, ingawa hakuna aliyejua ni nini. Mchuzi ukagawiwa watu, lakini walipoanza kula, wakalia, “Ee mtu wa Mungu, kuna mauti ndani ya chungu.” Nao hawakuweza kula.

4:41 Kut 15:25; 2Fal 2:21Elisha akasema, “Leteni unga.” Akauweka ndani ya chungu na kusema, “Wagawie watu ili wale.” Wala hapakuwa na kitu chochote chenye madhara ndani ya chungu.

Watu Mia Wanalishwa

4:42 1Sam 9:4; Mt 14:17Akaja mtu kutoka Baal-Shalisha, akimletea mtu wa Mungu mikate ishirini ya shayiri iliyookwa kutokana na nafaka ya kwanza, pamoja na masuke ya nafaka mpya. Elisha akasema, “Wape watu ili wale.”

4:43 Lk 9:13; Yn 6:12Mtumishi wake akamuuliza, “Nitawezaje kuandaa hii mbele ya watu mia?”

Lakini Elisha akajibu, “Wape watu ili wale. Kwa maana hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Watakula na kusaza.’ ” Basi akaiandaa mbele yao ile mikate, wakala na baadhi yake wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.

Read More of 2 Wafalme 4

2 Wafalme 5:1-27

Naamani Aponywa Ukoma

5:1 Mwa 10:22; Lk 4:27Wakati huu, Naamani alikuwa jemadari wa jeshi la mfalme wa Aramu. Alikuwa mtu mkuu mbele ya bwana wake na aliyeheshimiwa sana, kwa sababu kupitia kwake, Bwana alikuwa amewapa Aramu ushindi. Alikuwa askari shujaa, lakini alikuwa na ukoma.5:1 Ukoma ni neno lililotumika kwa Kiebrania kueleza magonjwa mbalimbali ya ngozi ambayo si lazima yawe ni ukoma halisi.

5:2 2Fal 6:23Siku hizo vikosi kutoka Aramu vilikuwa vimekwenda na vikawa vimemteka msichana kutoka Israeli, naye akamtumikia mkewe Naamani. 5:3 Mwa 20:7Akamwambia bibi yake, “Kama bwana wangu angelimwona nabii aliyeko Samaria! Angemponya ukoma wake.”

Naamani akaenda kwa bwana wake na kumwambia alichosema yule msichana kutoka Israeli. 5:5 Mwa 24:53; 1Sam 9:7Mfalme wa Aramu5:5 Yaani mfalme wa Shamu. akamjibu, “Hakika, nenda. Nitatuma barua kwa mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaondoka, akiwa amechukua talanta kumi5:5 Talanta 10 za fedha ni sawa na kilo 340. za fedha, shekeli 6,000 za dhahabu,5:5 Shekeli 6,000 za dhahabu ni sawa na kilo 70. na mivao kumi ya mavazi. Barua aliyopelekea mfalme wa Israeli iliandikwa hivi: “Pamoja na barua hii ninamtuma mtumishi wangu, Naamani, kwako ili uweze kumponya ukoma wake.”

5:7 Mwa 30:2; Kum 32:39; 1Fal 20:7Mara mfalme wa Israeli alipomaliza kuisoma ile barua, akararua mavazi yake na kusema, “Je, mimi ni Mungu? Je, mimi naweza kuua na kufufua tena? Kwa nini huyu mtu anamtuma mtu ili mimi nipate kumponya ukoma wake? Tazama jinsi anavyotafuta kuanzisha ugomvi nami!”

5:8 1Fal 22:7Elisha mtu wa Mungu aliposikia kwamba mfalme wa Israeli alikuwa amerarua mavazi yake, akamtumia ujumbe huu: “Kwa nini umerarua mavazi yako? Mwamuru mtu huyo aje kwangu, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaenda, akiwa na farasi zake na magari yake, na kusimama mlangoni mwa nyumba ya Elisha. 5:10 Yn 9:7; Law 14:7Elisha akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda uoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona, nawe utatakasika.”

5:11 Kut 7:19Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika, akasema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje, asimame na kuliitia jina la Bwana Mungu wake, na kuweka mkono wake juu ya mahali pagonjwa, aniponye ukoma wangu. 5:12 Mit 14:17, 29Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora zaidi kuliko mito yoyote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu.

5:13 2Fal 6:21Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, usingelifanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ” 5:14 Law 14:7; Ay 33:25Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo.

5:15 Yos 4:24; 1Sam 17:46Kisha Naamani na wahudumu wake wote wakarudi kwa yule mtu wa Mungu. Akasimama mbele yake na kusema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu katika ulimwengu wote isipokuwa katika Israeli. Tafadhali sasa upokee zawadi kutoka kwa mtumishi wako.”

5:16 Mwa 14:23; Dan 5:17Nabii akajibu, “Hakika kama Bwana aishivyo, ambaye ninamtumikia, sitapokea kitu hata kimoja.” Ingawa Naamani alimsihi sana, yeye alikataa.

5:17 Kut 20:24Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea, tafadhali mtumishi wako na apewe udongo kiasi cha mzigo wa kuweza kubebwa na punda wawili, kwa sababu mtumishi wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa na dhabihu kwa mungu mwingine isipokuwa Bwana. 5:18 2Fal 7:2Lakini Bwana na amsamehe mtumishi wake kwa kitu hiki kimoja: Wakati bwana wangu atakapoingia kwenye hekalu la Rimoni ili kusujudu, naye akiwa anauegemea mkono wangu, nami nikasujudu huko pia, wakati nitakaposujudu ndani ya hekalu la Rimoni, Bwana na amsamehe mtumishi wako kwa ajili ya jambo hili.”

5:19 1Sam 1:17; Mdo 15:33Elisha akamwambia, “Nenda kwa amani.”

Baada ya Naamani kusafiri umbali fulani, 5:20 Kut 20:7Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akajiambia mwenyewe, “Bwana wangu amemwachia kirahisi sana Naamani, huyu Mwaramu, kwa kutokupokea kutoka kwake vile alivyovileta. Hakika kama Bwana aishivyo, nitamkimbilia na kupata kitu kutoka kwake.”

Hivyo Gehazi akaharakisha kumfuatilia Naamani. Naamani alipomwona akikimbia kumwelekea, akashuka chini kutoka kwenye gari lake na kwenda kumlaki. Akauliza, “Je, mambo yote ni sawa?”

5:22 2Fal 5:5; Mwa 45:22Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa. Bwana wangu amenituma nikuambie, ‘Vijana wawili kutoka kwa wana wa manabii wamenijia kutoka nchi ya vilima ya Efraimu. Tafadhali wape talanta ya fedha5:22 Talanta ya fedha ni sawa na kilo 34. na mivao miwili ya mavazi.’ ”

Naamani akasema, “Hakika, chukua talanta mbili za fedha.” Akamsihi Gehazi azipokee, kisha akafunga talanta mbili za fedha katika mifuko miwili pamoja na mivao miwili ya mavazi. Akawapa watumishi wake wawili mizigo hiyo, nao wakaibeba wakitangulia mbele ya Gehazi. Gehazi alipofika kwenye kilima, akavichukua vile vitu kutoka kwa wale watumishi na kuvificha ndani ya nyumba. Akawaaga wale watu, nao wakaondoka. Kisha akaingia ndani na kusimama mbele ya Elisha bwana wake.

Elisha akamuuliza, “Gehazi, ulikuwa wapi?”

Gehazi akajibu, “Mtumishi wako hakwenda popote.”

5:26 2Fal 5:16; Yer 45:5Lakini Elisha akamwambia, “Je, roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati yule mtu aliposhuka kutoka kwenye gari lake ili kukulaki? Je, huu ni wakati wa kupokea fedha au kupokea nguo, mashamba ya mizeituni, mashamba ya mizabibu, makundi ya kondoo na mbuzi, makundi ya ngʼombe, au watumishi wa kiume na wa kike? 5:27 Hes 12:10; Kut 4:6Ukoma wa Naamani utakushika wewe na wazao wako milele.” Kisha Gehazi akaondoka mbele ya Elisha, mwenye ukoma, mweupe kama theluji.

Read More of 2 Wafalme 5

2 Wafalme 6:1-23

Shoka Laelea

6:1 1Sam 10:5Wana wa manabii wakamwambia Elisha, “Tazama, mahali hapa tunapokutana nawe ni padogo sana kwetu. Twendeni Yordani, mahali ambapo kila mmoja wetu anaweza kupata nguzo moja, nasi tujenge huko mahali petu pa kuishi.”

Naye akawaambia, “Nendeni.”

Kisha mmoja wao akasema, “Je, tafadhali, huwezi kufuatana na watumishi wako?”

Elisha akajibu, “Nitakuja.” Naye akaenda pamoja nao.

Basi wakaenda Yordani, nao wakaanza kukata miti. Mmoja wao alipokuwa anakata mti, shoka lilitumbukia kwenye maji. Akalia, “Ee bwana wangu, shoka lilikuwa la kuazima!”

6:6 Kut 15:25; 2Fal 2:21Mtu wa Mungu akauliza, “Je, liliangukia wapi?” Alipomwonyesha mahali penyewe, Elisha akakata kijiti na kukitupa mahali pale, nalo shoka likaelea. Akasema, “Lichukue.” Kisha yule mtu akanyoosha mkono wake, akalichukua.

Elisha Awanasa Waaramu Waliopofushwa

Wakati huo mfalme wa Aramu alikuwa akipigana vita na Israeli. Baada ya kukubaliana na maafisa wake, akasema, “Nitapiga kambi yangu mahali fulani na fulani.”

6:9 2Fal 6:12Mtu wa Mungu akatuma ujumbe kwa mfalme wa Israeli: “Jihadhari usije ukapita mahali pale, kwa sababu Waaramu wanashuka huko.” 6:10 Yer 11:18Kwa hiyo mfalme wa Israeli akatuma neno la tahadhari mahali pale alikokuwa ameelekezwa na mtu wa Mungu. Mara kwa mara Elisha alimwonya mfalme kwamba watu wawe macho kwenye maeneo kama hayo.

Hili lilimfadhaisha sana mfalme wa Aramu. Akawaita maafisa wake, akawauliza, “Je, hamtaniambia ni nani miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?”

6:12 2Fal 6:9Mmoja wa maafisa wake akasema, “Mfalme bwana wangu, hakuna hata mmoja wetu. Lakini Elisha, yule nabii aliye Israeli, humwambia mfalme wa Israeli hata yale maneno unayozungumza katika chumba chako cha kulala.”

6:13 Mwa 37:17Mfalme akaagiza akisema, “Nendeni, mkatafute aliko, ili niweze kutuma watu kumkamata.” Taarifa ikarudi kwamba, “Yuko Dothani.” 6:14 2Fal 1:9Ndipo akatuma farasi na magari ya vita na jeshi lenye nguvu huko. Walikwenda usiku na kuuzunguka mji.

Kesho yake asubuhi na mapema, mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi, pamoja na farasi na magari ya vita, likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu, bwana wangu! Tutafanya nini?”

6:16 2Nya 32:7; Za 55:18Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi zaidi kuliko wale walio pamoja nao.”

Kisha Elisha akaomba, “Ee Bwana, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo Bwana akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya moto, yamemzunguka Elisha pande zote.

6:18 Mwa 19:11; Mdo 13:11Wakati adui waliposhuka kumwelekea, Elisha akamwomba Bwana: “Wapige watu hawa kwa upofu.” Basi Mungu akawapiga kwa upofu, kama Elisha alivyoomba.

Elisha akawaambia, “Hii sio njia yenyewe, na huu sio huo mji. Nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa huyo mtu mnayemtafuta.” Naye akawapeleka Samaria.

Baada ya kuingia mjini, Elisha akasema, “Bwana, yafungue macho ya watu hawa ili wapate kuona.” Ndipo Bwana akayafungua macho yao, na walipotazama, kumbe hapo ndipo walipojikuta, ndani ya Samaria.

6:21 2Fal 5:13Wakati mfalme wa Israeli alipowaona, akamuuliza Elisha, “Je, baba yangu, niwaue?”

6:22 Kum 20:11; 2Nya 28:8-15Naye akajibu, “Usiwaue. Je, utawaua watu uliowateka kwa upanga wako mwenyewe na upinde wako? Wape chakula na maji ili wapate kula na kunywa, na kisha wamrudie bwana wao.” 6:23 2Fal 5:2Basi akawaandalia karamu kubwa, na baada ya kula na kunywa, akawaaga nao wakarudi kwa bwana wao. Hivyo, vikosi kutoka Aramu vikakoma kuvamia nchi ya Israeli.

Read More of 2 Wafalme 6