Ufunuo 19 – Kiswahili Contemporary Version NEN

Kiswahili Contemporary Version

Ufunuo 19:1-21

Shangwe Huko Mbinguni

119:1 Ufu 11:15; 7:10; 4:11Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipiga kelele wakisema:

“Haleluya!

Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu,

219:2 Kum 32:43; Ufu 6:10kwa maana hukumu zake

ni za kweli na za haki.

Amemhukumu yule kahaba mkuu

aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake.

Mungu amemlipiza kisasi

kwa ajili ya damu ya watumishi wake.”

319:3 Isa 34:10; Ufu 14:11Wakasema tena kwa nguvu:

“Haleluya!

Moshi wake huyo kahaba unapanda juu

milele na milele.”

419:4 Ufu 4:4-6; 5:14Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu:

“Amen, Haleluya!”

519:5 Za 134:1; Ufu 11:18Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema:

“Msifuni Mungu wetu,

ninyi watumishi wake wote,

ninyi nyote mnaomcha,

wadogo kwa wakubwa!”

619:6 Ufu 11:15Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema:

“Haleluya!

Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anatawala.

719:7 Mt 25:10; Efe 5:32; Ufu 21:2, 9Tufurahi, tushangilie

na kumpa utukufu!

Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia

na bibi arusi wake amejiweka tayari.

819:8 Ufu 15:4; 19:14; 15:6; Isa 61:10; Eze 44:17; Zek 3:4Akapewa kitani safi, nyeupe

inayongʼaa, ili avae.”

(Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.)

919:9 Ufu 1:19; Lk 14:15; Ufu 21:5; 22:6Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”

1019:10 Ufu 22:8; Mdo 10:25, 26; Ufu 22:9; 12:17Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.”

Aliyepanda Farasi Mweupe

1119:11 Ufu 6:2; 3:14; Kut 15:3Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita. 1219:12 Ufu 1:14; 6:2; 2:17Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe. 1319:13 Isa 63:2, 3; Yn 1:1Amevaa joho lililochoviwa katika damu, na Jina lake ni “Neno la Mungu.” 1419:14 Ufu 19:8; 3:4; 17:14Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri. 1519:15 Ufu 1:16; 12:5; 14:20; Isa 11:4; 2The 2:8; Za 2:9Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi. 1619:16 Ufu 17:14; 19:12; 1Tim 6:15Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili:

Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.

Mnyama Na Majeshi Yake Yashindwa

1719:17 Ufu 8:13; Eze 39:17Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njooni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu, 1819:18 Eze 39:18-20ili mpate kula nyama ya wafalme na ya majemadari, ya mashujaa, ya farasi na ya wapanda farasi, nyama ya wanadamu, wote walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”

1919:19 Ufu 16:14, 16Kisha nikamwona yule mnyama na wafalme wa dunia pamoja na majeshi yao wakiwa wamekusanyika pamoja ili kufanya vita dhidi ya yule aliyempanda farasi pamoja na jeshi lake. 2019:20 Ufu 16:13; 13:12; Dan 7:11; Ufu 21:8; 14:19Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti. 21Wale waliosalia waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule aliyekuwa amempanda farasi nao ndege wote wakajishibisha kwa nyama yao.