2 Wafalme 20 – Kiswahili Contemporary Version NEN

Kiswahili Contemporary Version

2 Wafalme 20:1-21

Ugonjwa Wa Hezekia

(2 Nyakati 32:24-26; Isaya 38:1-8, 21-22)

1Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”

2Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana: 320:3 Mwa 8:1; 2Nya 31:20“Ee Bwana, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.

4Kabla Isaya hajaondoka katika ua wa kati, neno la Bwana likamjia, akaambiwa: 520:5 1Fal 9:3; Za 39:12“Rudi ukamwambie Hezekia, kiongozi wa watu wangu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako; nitakuponya. Siku ya tatu kuanzia sasa utapanda kwenda Hekalu la Bwana. 620:6 2Fal 19:34; 1Nya 17:19Nitakuongezea miaka kumi na mitano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi!’ ”

7Kisha Isaya akasema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini.” Wakafanya hivyo na kuiweka kwenye jipu, naye akapona.

8Hezekia alikuwa amemuuliza Isaya, “Kutakuwa na ishara gani kwamba Bwana ataniponya mimi, na kwamba nitapanda kwenda Hekalu la Bwana siku ya tatu tangu leo?”

920:9 Kum 13:2; Yer 44:29Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara ya Bwana kwako kwamba Bwana atafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?”

1020:10 2Fal 3:18Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.”

1120:11 Yos 10:13; 2Nya 32:31Ndipo nabii Isaya akamwita Bwana, naye Bwana akakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.

Wajumbe Kutoka Babeli

(Isaya 39:1-8)

12Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia. 13Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonyesha vitu vyote vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina zake. Hapakuwa na kitu chochote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha.

14Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?”

Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kutoka Babeli.”

15Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”

Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu chochote katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.”

16Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana: 1720:17 2Fal 24:13; Yer 52:17-23Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana. 1820:18 2Fal 24:15; Mik 4:10Nao baadhi ya wazao wako, nyama yako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mbali, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”

19Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Bwana ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Lakini si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?”

20Matukio mengine ya utawala wa Hezekia, mafanikio yake yote, na jinsi alivyotengeneza bwawa na mfereji ambao ulileta maji katika mji, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 21Hezekia akafa, akazikwa pamoja na baba zake. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.