2 Wafalme 15 – Kiswahili Contemporary Version NEN

Kiswahili Contemporary Version

2 Wafalme 15:1-38

Azaria Mfalme Wa Yuda

(2 Nyakati 26)

115:1 2Fal 14:21Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Azaria mwana wa Amazia mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na miwili. Mama yake aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. 3Akatenda yaliyo mema machoni pa Bwana, kama Amazia baba yake alivyofanya. 4Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.

515:5 Law 13:46; Mwa 41:40Bwana akampiga mfalme kwa ukoma mpaka siku aliyokufa, naye aliishi katika nyumba iliyotengwa peke yake. Yothamu mwana wa mfalme akawa msimamizi wa jumba la mfalme, na akawatawala watu wa nchi.

6Matukio mengine ya utawala wa Azaria na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 715:7 Isa 6:1Azaria akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa karibu nao katika Mji wa Daudi, na Yothamu mwanawe akawa mfalme baada yake.

Zekaria Mfalme Wa Israeli

8Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Zekaria mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miezi sita. 9Akafanya maovu machoni pa Bwana, kama baba zake walivyofanya. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.

1015:10 2Fal 12:20Shalumu mwana wa Yabeshi akafanya shauri baya dhidi ya Zekaria. Akamshambulia mbele ya watu, akamuua na kuingia mahali pake kuwa mfalme. 11Matukio mengine ya utawala wa Zekaria yameandikwa kwenye kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. 1215:12 2Fal 10:30Kwa hiyo neno la Bwana lililonenwa kwa Yehu likatimia, kwamba, “Wazao wako wataketi juu ya kiti cha enzi cha Israeli hadi kizazi cha nne.”

Shalumu Mfalme Wa Israeli

13Shalumu mwana wa Yabeshi akawa mfalme katika mwaka wa thelathini na tisa wa Uzia mfalme wa Yuda, naye akatawala katika Samaria kwa mwezi mmoja. 1415:14 1Fal 15:33; 2Fal 12:20Kisha Menahemu mwana wa Gadi akaenda kutoka Tirsa mpaka Samaria. Akamshambulia Shalumu mwana wa Yabeshi huko Samaria, akamuua na kuingia mahali pake kuwa mfalme.

15Matukio mengine ya utawala wa Shalumu, na mauaji aliyoyafanya, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.

1615:16 2Fal 8:12; Hos 13:16Wakati ule, akianzia Tirsa, Menahemu alishambulia Tifsa na kila mtu ndani yake, na wale waliokuwa maeneo jirani, kwa sababu walikataa kufungua malango yao. Akaiangamiza Tifsa yote, na kuwapasua matumbo wanawake wote wenye mimba.

Menahemu Mfalme Wa Israeli

17Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi akawa mfalme wa Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka kumi. 18Akatenda maovu machoni pa Bwana. Katika wakati wa utawala wake wote, hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.

1915:19 1Nya 5:6, 26Kisha Pulu mfalme wa Ashuru akaishambulia Israeli. Menahemu mfalme wa Israeli akampa talanta elfu moja za fedha15:19 Talanta 1,000 za fedha ni sawa na tani 34. ili amsaidie na kumwezesha katika utawala wake. 2015:20 2Fal 12:18Menahemu akatoza fedha hizi kwa nguvu kutoka kwa Israeli. Kila mtu tajiri alilazimika kuchanga shekeli hamsini za fedha15:20 Shekeli 50 za fedha ni sawa na gramu 600. ambazo alipewa mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akajiondoa na hakuendelea kuikalia nchi.

21Matukio mengine ya utawala wa Menahemu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 22Menahemu akalala pamoja na baba zake. Naye Pekahia mwanawe akawa mfalme baada yake.

Pekahia Mfalme Wa Israeli

23Katika mwaka wa hamsini wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, akatawala miaka miwili. 24Pekahia akafanya uovu machoni pa Bwana. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda. 2515:25 2Nya 28:6; Isa 7:1Mmoja wa maafisa wake wakuu, Peka mwana wa Remalia, akafanya shauri baya dhidi yake. Akachukua watu hamsini wa Gileadi pamoja naye, akamuua Pekahia, pamoja na Argobu na Aria, katika ngome ya jumba la kifalme huko Samaria. Kwa hiyo Peka akamuua Pekahia, naye akaingia mahali pake kuwa mfalme.

26Matukio mengine ya utawala wa Pekahia na yote aliyoyafanya yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.

Peka Mfalme Wa Israeli

2715:27 2Nya 28:6; Isa 7:4Katika mwaka wa hamsini na mbili wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Peka mwana wa Remalia akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, naye alitawala miaka ishirini. 28Akafanya maovu machoni pa Bwana. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.

2915:29 1Nya 5:26; Yer 50:17; Isa 14:6, 17Wakati wa utawala wa Peka mfalme wa Israeli, Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru alikuja na kuteka Iyoni, Abel-Beth-Maaka, Yanoa, Kedeshi na Hazori. Akateka miji ya Gileadi na Galilaya, pamoja na nchi yote ya Naftali, na kuwahamishia watu wote Ashuru. 3015:30 2Fal 17:1Kisha Hoshea mwana wa Ela akafanya shauri baya dhidi ya Peka mwana wa Remalia. Akamshambulia na kumuua, kisha akaingia mahali pake kuwa mfalme katika mwaka wa ishirini wa Yothamu mwana wa Uzia.

31Matukio mengine ya utawala wa Peka na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?

Yothamu Mfalme Wa Yuda

(2 Nyakati 27)

3215:32 1Nya 5:17Katika mwaka wa pili wa utawala wa Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli, Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala. 33Alikuwa na miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki. 3415:34 1Fal 14:8Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya. 35Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu la Bwana.

36Matukio mengine ya utawala wa Yothamu na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 3715:37 2Fal 16:5(Katika siku hizo, Bwana akaanza kuwatuma Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia dhidi ya Yuda.) 38Yothamu akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi, mji wa baba zake. Naye Ahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.