2 Wafalme 10 – Kiswahili Contemporary Version NEN

Kiswahili Contemporary Version

2 Wafalme 10:1-36

Jamii Ya Ahabu Yauawa

110:1 1Fal 13:32; Amu 8:30Wakati huu katika Samaria walikuwepo wana sabini wa nyumba ya Ahabu. Kwa hiyo Yehu akaandika barua na kuzituma Samaria: kwa maafisa wa Yezreeli, kwa wazee, na kwa walezi wa watoto wa Ahabu. Akasema, 2“Mara tu barua hii itakapokufikia, kwa kuwa wana wa bwana wako wapo pamoja nawe, nawe una magari ya vita na farasi, mji wenye ngome na silaha, 3mchague mwenye uwezo zaidi kati ya wana wa bwana wako, na umweke juu ya kiti cha enzi cha baba yake. Kisha upigane kwa ajili ya nyumba ya bwana wako.”

4Lakini wakaogopa sana na kusema, “Ikiwa wafalme wawili hawakuweza kupambana na Yehu, sisi tutawezaje?”

510:5 Yos 9:8Basi msimamizi wa jumba la mfalme, mtawala wa mji, na wazee na walezi wakatuma ujumbe huu kwa Yehu: “Sisi tu watumishi wako, na tutafanya kila kitu utakachosema. Hatutamteuwa mtu yeyote kuwa mfalme. Wewe fanya uonalo kuwa ni bora.”

6Kisha Yehu akawaandikia barua ya pili, akisema, “Ikiwa ninyi mko upande wangu na mtanitii mimi, twaeni vichwa vya wana wa bwana wenu, na mnijie huku Yezreeli kesho wakati kama huu.”

Wakati huo wana sabini wa mfalme walikuwa wakiishi pamoja na viongozi wa mji wa Samaria, waliokuwa wakiwalea. 710:7 1Fal 21:21; 2Sam 4:8Hiyo barua ilipowafikia, watu hawa wakawachukua wale wana sabini wa mfalme na kuwachinja wote. Wakaweka vichwa vyao ndani ya makapu na kumpelekea Yehu huko Yezreeli. 8Mjumbe alipofika, akamwambia Yehu, “Wameleta vichwa vya wana wa mfalme.”

Ndipo Yehu akaagiza, “Viwekeni malundo mawili katika ingilio la lango la mji mpaka asubuhi.”

9Asubuhi yake, Yehu akatoka nje. Akasimama mbele ya watu wote na akasema, “Hamna hatia. Ni mimi niliyefanya shauri baya dhidi ya bwana wangu na kumuua, lakini ni nani aliyewaua wote hawa? 1010:10 2Fal 9:7-10; 1Fal 21:29Fahamuni basi kwamba, hakuna neno ambalo Bwana amesema dhidi ya nyumba ya Ahabu ambalo halitatimia. Bwana amefanya lile aliloahidi kupitia mtumishi wake Eliya.” 11Hivyo Yehu akaua kila mtu huko Yezreeli aliyekuwa amebaki wa nyumba ya Ahabu, ikiwa ni pamoja na wakuu wake, rafiki zake wa karibu, na makuhani wake. Hakuacha yeyote anusurike.

12Kisha Yehu akaondoka kuelekea Samaria. Alipokuwa njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya ya kondoo, yaani, Beth-Ekedi ya wachunga kondoo, 1310:13 2Fal 8:29; 2Nya 22:8Yehu akakutana na watu wa jamaa ya Ahazia mfalme wa Yuda, akauliza, “Ninyi ni nani?”

Wao wakasema, “Sisi ni jamaa ya Ahazia, nasi tumeshuka kuwasalimu jamaa ya mfalme na ya mama malkia.”

1410:14 2Fal 10:11Yehu akaagiza, “Wakamateni wakiwa hai!” Kwa hiyo wakawachukua wakiwa hai, watu arobaini na wawili, na kuwachinja kando ya kisima cha Beth-Ekedi. Hakuacha yeyote anusurike.

1510:15 Yer 35:6, 14-19; 1Nya 2:55; Ezr 10:19Baada ya kuondoka hapo, alimkuta Yehonadabu mwana wa Rekabu, aliyekuwa akienda kumlaki. Yehu akamsalimu na kusema, “Je, moyo wako ni mnyofu kwangu kama moyo wangu ulivyo kwako?”

Yehonadabu akajibu, “Ndiyo.”

Yehu akasema, “Kama ndivyo, nipe mkono wako.” Yeye akampa mkono, naye Yehu akampandisha kwenye gari lake la vita. 1610:16 Hes 25:13Yehu akasema, “Twende pamoja ukaone wivu wangu kwa ajili ya Bwana.” Hivyo wakasafiri pamoja kwenye gari lake.

1710:17 2Fal 9:8Yehu alipofika Samaria, akawaua wale wote waliokuwa wamesalia wa jamaa ya Ahabu, akawaangamiza, sawasawa na neno la Bwana alilosema kupitia Eliya.

Watumishi Wa Baali Wauawa

1810:18 Amu 2:11Kisha Yehu akawaleta watu wote pamoja na kuwaambia, “Ahabu alimtumikia Baali kidogo. Lakini Yehu atamtumikia zaidi. 1910:19 1Fal 18:19Sasa waiteni manabii wote wa Baali, watumishi wake wote na makuhani wake wote. Hakikisheni kwamba hakuna hata mmoja atakayekosekana, kwa sababu ninakwenda kutoa kafara kubwa sana kwa Baali. Yeyote atakayeshindwa kuja hataendelea kuishi.” Lakini Yehu alifanya hivyo kwa hila ili apate kuwaangamiza watumishi wote wa Baali.

2010:20 Kut 32:5Yehu akasema, “Itisheni kusanyiko kwa heshima ya Baali.” Basi wakatangaza jambo hilo. 21Kisha Yehu akapeleka ujumbe katika Israeli yote, nao watumishi wote wa Baali wakaja, hakuna hata mmoja ambaye hakufika. Wakasongana ndani ya hekalu la Baali hadi likajaa tangu mlango hadi mwisho wake. 22Naye Yehu akamwambia yule aliyekuwa mtunza chumba cha mavazi, “Leta majoho kwa ajili ya watumishi wote wa Baali.” Basi akawaletea majoho.

23Kisha Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu wakaingia ndani ya hekalu la Baali. Yehu akawaambia watumishi wa Baali, “Tazameni kila mahali mhakikishe kwamba hakuna hata mtumishi mmoja wa Bwana aliye hapa pamoja nanyi, ila ni watumishi wa Baali tu.” 2410:24 Yos 2:14Kwa hiyo wakaingia ndani ili kutoa kafara na sadaka ya kuteketezwa. Wakati huu, Yehu alikuwa amewaweka watu wake themanini akiwa amewapa onyo kwamba, “Ikiwa mmoja wenu atamwachia mtu yeyote ninayemweka mikononi mwake atoroke, itakuwa uhai wako kwa uhai wake.”

2510:25 Kut 22:20; 1Fal 18:40Mara baada ya Yehu kutoa sadaka ya kuteketezwa, akawaamuru walinzi na maafisa: “Ingieni ndani, waueni; asitoroke hata mmoja.” Basi wakawakatakata kwa upanga. Walinzi na maafisa wakazitupa zile maiti nje, kisha wakaingia mahali pa ndani pa kuabudia miungu katika hekalu la Baali. 2610:26 Kut 23:24Wakaileta ile nguzo ya kuabudiwa nje ya hekalu la Baali, na wakaichoma moto. 27Wakabomoa ile nguzo ya kuabudiwa ya Baali pamoja na hekalu la Baali, nao watu wakapafanya kuwa choo hadi leo.

28Kwa hiyo Yehu akaangamiza kuabudiwa kwa Baali katika Israeli. 2910:29 1Fal 12:30; Kut 32:4Hata hivyo, Yehu hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda, yaani kuabudu ndama za dhahabu huko Betheli ya Dani.

3010:30 2Fal 15:12Bwana akamwambia Yehu, “Kwa kuwa umefanya vyema kwa kutimiza yaliyo sawa machoni pangu, na umetenda kwa nyumba ya Ahabu yale yote niliyokuwa nimekusudia kutenda, wazao wako wataketi juu ya kiti cha enzi cha Israeli hadi kizazi cha nne.” 3110:31 Kum 4:9; Mit 4:23Lakini Yehu hakuwa mwangalifu kushika sheria za Bwana, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda.

3210:32 Za 107:39Katika siku hizo, Bwana akaanza kupunguza ukubwa wa Israeli. Hazaeli akawashinda Waisraeli sehemu zote za nchi yao 3310:33 Hes 32:34; Isa 17:2mashariki ya Yordani, katika nchi yote ya Gileadi (eneo la Gadi, Reubeni na Manase), kutoka Aroeri karibu na Bonde la Arnoni kupitia Gileadi hadi Bashani.

34Kwa matukio mengine ya utawala wa Yehu, yote aliyofanya na mafanikio yake yote, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?

35Yehu akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa huko Samaria. Naye Yehoahazi mwanawe akawa mfalme baada yake. 36Muda Yehu aliotawala juu ya Israeli huko Samaria ilikuwa miaka ishirini na minane.