2 Samweli 19 – Kiswahili Contemporary Version NEN

Kiswahili Contemporary Version

2 Samweli 19:1-43

Yoabu Amkemea Mfalme

1Yoabu akaambiwa, “Mfalme analia na kumwombolezea Absalomu.” 2Kwa jeshi lote, ushindi wa siku ile ukageuka kuwa maombolezo, kwa sababu siku ile vikosi vilisikia ikisemwa, “Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe.” 3Siku ile watu wakaingia mjini kimya kama vile waingiavyo kwa aibu watu waliokimbia kutoka vitani. 419:4 2Sam 15:30; 18:33; 1Sam 4:12Mfalme akafunika uso wake akalia kwa sauti, akisema, “Ee mwanangu Absalomu! Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!”

5Kisha Yoabu akaingia ndani ya nyumba ya mfalme na kusema, “Leo umewaaibisha watu wako wote, waliookoa maisha yako, maisha ya wanao na binti zako, maisha ya wake zako na masuria wako. 6Unawapenda wale wanaokuchukia, na unawachukia wale wanaokupenda. Leo umeonyesha wazi kwamba majemadari wako na watu wao hawana maana kwako. Naona kwamba ungefurahi kama Absalomu angekuwa hai leo na sisi sote tuwe tumekufa. 719:7 Mit 14:28Sasa utoke nje ukawatie moyo watu wako. Naapa kwa Bwana kwamba ikiwa hutatoka nje, hakuna mtu atakayesalia pamoja nawe ifikapo leo jioni. Hii itakuwa mbaya zaidi kwako kuliko maafa yote yaliyokupata tangu ujana wako hadi sasa.”

819:8 2Sam 15:2; Rut 4:1; 2Sam 18:4, 24; 2Fal 14:12; 1Fal 12:16Kwa hiyo mfalme akaondoka akaketi kitini pake penye lango. Watu walipoambiwa, “Mfalme ameketi langoni,” watu wote wakamjia.

Daudi Arudi Yerusalemu

Wakati huo, Waisraeli walikuwa wamekimbilia nyumbani kwao. 919:9 2Sam 8:1-14; 15:14; 5:18; 1Sam 17:1; 18:1Katika makabila yote ya Israeli, watu walikuwa wanabishana wao kwa wao, wakisema, “Mfalme alituokoa kutoka mikononi mwa adui zetu; ndiye alituokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti. Lakini sasa mfalme ameikimbia nchi kwa sababu ya Absalomu, 10naye Absalomu, tuliyemtia mafuta atutawale, amekufa vitani. Basi mbona hamsemi lolote kuhusu kumrudisha mfalme?”

1119:11 2Sam 15:24Mfalme Daudi akapeleka ujumbe huu kwa makuhani Sadoki na Abiathari, kusema: “Waulizeni wazee wa Yuda, ‘Kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme katika jumba lake la kifalme, maadamu kile kinachosemwa katika Israeli yote kimemfikia mfalme katika makao yake? 1219:12 Mwa 2:23; Amu 9:2; 2Sam 5:1Ninyi ni ndugu zangu, nyama yangu na damu yangu mwenyewe. Kwa hiyo kwa nini mwe wa mwisho kumrudisha mfalme?’ 1319:13 2Sam 17:25; Mwa 29:14; Rut 1:17; 2Sam 2:13; 1Fal 8:16; 1Nya 2:16; 17:12, 18; 1Fal 19:2Nanyi mwambieni Amasa, ‘Je, wewe si nyama yangu mwenyewe na damu yangu? Mungu na anishughulikie, tena kwa ukali, kama kuanzia sasa na kuendelea wewe si jemadari wa jeshi langu mahali pa Yoabu.’ ”

1419:14 Amu 20:1; Za 110:2-3; Mdo 4:32Aliipata mioyo ya watu wote wa Yuda kama vile walikuwa mtu mmoja. Wakapeleka ujumbe kwa mfalme, kusema, “Rudi, wewe na watu wako wote.” 1519:15 1Sam 11:15; Yos 5:9Ndipo mfalme akarudi, akaenda hadi kufikia Mto Yordani.

Basi watu wa Yuda walikuwa wamekuja mpaka Gilgali ili kutoka kwenda kumlaki mfalme na kumvusha Mto Yordani. 1619:16 2Sam 16:5-13; 1Fal 2:8Shimei mwana wa Gera, wa kabila la Benyamini kutoka Bahurimu, akaharakisha kuteremka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki Mfalme Daudi. 1719:17 2Sam 9:2; Mwa 43:16; 2Sam 16:1-2Pamoja naye walikuwepo Wabenyamini elfu moja wakiwa wamefuatana na Siba, msimamizi wa nyumba ya Sauli, pia wanawe kumi na watano, na watumishi ishirini. Wakaharakisha kwenda Yordani, mahali mfalme alipokuwa. 18Wakavuka kivuko ili kuwachukua watu wa nyumbani mwa mfalme ili kuwavusha na kufanya kila kitu alichotaka.

Shimei mwana wa Gera alipovuka Yordani, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme, 1919:19 2Sam 16:6-8; 1Sam 22:13; Za 32:2; Rum 4:6-8; 2Kor 5:19; Mit 28:13; Mt 5:25; 2Sam 16:5-6; 13:33na kumwambia, “Bwana wangu na asinihesabie hatia. Usikumbuke jinsi mtumishi wako alivyofanya kosa siku ile bwana wangu mfalme alipoondoka Yerusalemu. Mfalme aliondoe moyoni mwake. 2019:20 2Sam 16:5Kwa maana mimi mtumishi wako najua nimefanya dhambi, lakini leo nimekuja hapa kama wa kwanza wa nyumba yote ya Yosefu kushuka na kumlaki bwana wangu mfalme.”

2119:21 1Sam 26:6; Kut 22:28; 1Sam 12:3; 26:9; 2Sam 16:7-8; Mhu 10:20; Mdo 23:5; 2Pet 2:10-11; Yud 8Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, Shimei hapaswi kuuawa kwa ajili ya hili? Alimlaani mpakwa mafuta wa Bwana.”

2219:22 2Sam 2:18; 16:10; 1Sam 11:13; 16:8; Mt 8:29Daudi akajibu, “Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya? Leo hii mmekuwa adui zangu! Je, leo kuna yeyote atakayeuawa katika Israeli? Je, mimi sijui kuwa leo ndimi mfalme katika Israeli yote?” 2319:23 1Fal 2:8, 42Basi mfalme akamwambia Shimei, “Hutakufa.” Naye mfalme akamwahidi kwa kiapo.

2419:24 2Sam 4:4; 9:6-10Pia Mefiboshethi mwana wa Sauli akashuka kwenda kumlaki mfalme. Hakuwa amenawa miguu wala kunyoa ndevu zake wala kufua nguo zake tangu siku mfalme alipoondoka Yerusalemu mpaka siku aliporudi ile salama. 2519:25 2Sam 16:17Wakati alipotoka Yerusalemu kuja kumlaki mfalme, mfalme akamuuliza, “Mefiboshethi, kwa nini hukufuatana nami?”

2619:26 Law 21:18; 2Sam 9:2Akasema, “Bwana wangu mfalme, maadamu mimi mtumishi wako ni kiwete, nilisema, ‘Nitandikiwe punda wangu, nimpande, ili niweze kwenda pamoja na mfalme.’ Lakini Siba mtumishi wangu akanisaliti. 2719:27 1Sam 29:9; 2Sam 14:17-20; 16:3; Za 15:3; 63:11; Mit 21:6; 26:28; Yer 9:4-5Naye amemchongea mtumishi wako kwa bwana wangu mfalme. Bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu, kwa hiyo fanya lolote linalokupendeza. 2819:28 1Sam 25:2; 2Sam 17:27; 9:7-13Wazao wote wa baba yangu hawastahili kitu kingine isipokuwa kifo kutoka kwa bwana wangu mfalme, lakini ulimpa mtumishi wako nafasi miongoni mwa wale waliokula mezani pako. Je, ninayo haki gani kumwomba mfalme zaidi ya hayo?”

2919:29 Kum 19:16-21; Za 82:2; 101:1-8; Mit 29:4Mfalme akamwambia, “Kwa nini useme zaidi? Naamuru wewe na Siba mgawanye mashamba.”

30Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu achukue kila kitu, kwa kuwa sasa bwana wangu mfalme amerudi nyumbani salama.”

3119:31 Za 90:10; 2Nya 35:25; Ezr 2:65; Mhu 2:8; 12:1; 2Sam 15:33; 1Fal 2:7; Neh 7:63Barzilai, Mgileadi, pia akashuka kutoka Rogelimu ili kuvuka Yordani pamoja na mfalme na kumsindikiza kutoka huko. 3219:32 2Sam 17:27Basi Barzilai alikuwa mzee sana mwenye umri wa miaka themanini. Alikuwa amempatia mfalme mahitaji wakati alipokuwa anaishi huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa mtu tajiri sana. 33Mfalme akamwambia Barzilai, “Vuka pamoja nami na ukae nami huko Yerusalemu, nami nitakupatia mahitaji yako.”

3419:34 Mwa 47:9; Za 39:4-5; Yak 4:14Lakini Barzilai akamjibu mfalme, “Je, nitaishi miaka mingine mingapi, hata nipande kwenda Yerusalemu pamoja na mfalme? 3519:35 Mwa 49:29; Yer 41:17; 1Fal 2:7; Za 90:10; Mhu 12:3-6Sasa nina miaka themanini. Je, naweza kutofautisha kati ya lililo jema na lililo baya? Je, mtumishi wako anaweza kujua ladha ya kile anachokula au anachokunywa? Je, bado naweza kusikiliza sauti za waimbaji wa kiume na za wanawake? Kwa nini mtumishi wako aongeze mzigo kwa bwana wangu mfalme? 36Mtumishi wako atavuka Yordani pamoja na mfalme kwa umbali mfupi tu, lakini kwa nini mfalme anizawadie kwa namna hii? 3719:37 Mwa 49:29; Yer 41:17; 1Fal 2:7Mruhusu mtumishi wako arudi, ili mimi nikafie katika mji wangu mwenyewe karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu. Lakini yupo hapa mtumishi wako Kimhamu. Mruhusu avuke pamoja na bwana wangu mfalme. Mtendee lolote linalokupendeza.”

38Mfalme akamwambia Barzilai, “Kimhamu atavuka Yordani pamoja nami, nami nitamtendea lolote litakalokupendeza. Nawe kitu chochote unachotaka kutoka kwangu nitakutendea.”

3919:39 Mwa 47:7; 31:55; 14:19; Kut 39:43; Yos 22:6; 1Sam 2:20Kwa hiyo watu wote wakavuka Yordani, kisha mfalme akavuka. Mfalme akambusu Barzilai na kumbariki; Barzilai akarudi nyumbani kwake.

40Mfalme alipovuka kwenda Gilgali, Kimhamu akavuka pamoja naye. Vikosi vyote vya Yuda na nusu ya vikosi vya Israeli vilimvusha mfalme.

4119:41 Amu 8:1; 12:1; 2Sam 19:15Baada ya kitambo kidogo watu wote wa Israeli wakaja kwa mfalme na kumwambia, “Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda, wamemrudisha mfalme kwa siri bila kutushirikisha, na kumvusha ngʼambo ya Yordani, yeye na nyumba yake, pamoja na watu wake wote?”

4219:42 2Sam 19:12; Rut 4:12; 1Nya 2:3-15; Za 78:68-70Watu wote wa Yuda wakawajibu watu wa Israeli, “Tulifanya hivi kwa sababu mfalme ni jamaa yetu wa karibu. Kwa nini mnakasirikia jambo hili? Je, tumekula kitu chochote cha mfalme? Je, tumejichukulia kitu chochote kwa ajili yetu wenyewe?”

4319:43 2Sam 5:1; 1Fal 11:30-31Ndipo watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, “Tunayo haki mara kumi kwa mfalme; sisi tunahusika zaidi na Daudi kuliko ninyi. Kwa nini basi mnatudharau? Je, hatukuwa wa kwanza kuzungumza kuhusu kumrudisha mfalme nyumbani?”

Lakini watu wa Yuda wakajibu kwa ukali hata zaidi kuliko watu wa Israeli.