2 Nyakati 26 – Kiswahili Contemporary Version NEN

Kiswahili Contemporary Version

2 Nyakati 26:1-23

Uzia Mfalme Wa Yuda

(2 Wafalme 14:21-22; 15:1-7)

126:1 1Fal 14:21; 2Nya 22:1Kisha watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, nao wakamfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake. 2Ndiye alijenga upya Elathi kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala pamoja na baba zake.

3Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na miwili. Mama yake aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. 4Akatenda yaliyo mema machoni pa Bwana, kama Amazia baba yake alivyofanya. 526:5 2Nya 15:2; Mwa 41:15; Dan 1:17; 2Nya 7:2; Dan 2:9; 10:1Akamtafuta Mungu katika siku za Zekaria, aliyemwelekeza kumcha Mungu. Wakati wote alipomtafuta Bwana, Mungu alimfanikisha.

626:6 Isa 2:6; Yer 25:20; Amo 3:9; Isa 14:29; 1Nya 21:16Alipigana vita dhidi ya Wafilisti na kubomoa kuta za Gathi, Yabne na Ashdodi. Kisha akajenga upya miji karibu na Ashdodi na mahali pengine katikati ya Wafilisti. 726:7 2Nya 21:16; 1Nya 5:20; 2Nya 20:1; 14:11; Mdo 26:22Mungu akamsaidia dhidi ya Wafilisti na dhidi ya Waarabu walioishi Gur-Baali na dhidi ya Wameuni. 826:8 Mwa 19:38; 2Nya 17:11; 1Sam 11:1; 2Sam 8:2Waamoni wakamletea Uzia ushuru, umaarufu wake ukaenea hadi kwenye mpaka wa Misri, kwa sababu alikuwa amekuwa na nguvu sana.

926:9 2Fal 14:13; 2Nya 25:23; Neh 2:13; 3:13; Zek 14:10Uzia akajenga minara huko Yerusalemu katika Lango la Pembeni, katika Lango la Bondeni na katika pembe, mahali kuta zikutanapo, kisha akaijengea ngome. 1026:10 2Nya 21:16Akajenga pia minara jangwani na kuchimba visima vingi vya maji, kwa sababu alikuwa na mifugo mingi chini ya vilimani na kwenye nchi tambarare. Alikuwa na watu wanaofanya kazi katika mashamba yake na kwenye mashamba yake ya mizabibu huko vilimani na katika ardhi zenye rutuba, kwa kuwa aliupenda udongo.

11Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililofunzwa vizuri, lililokuwa tayari kwenda vitani kwa vikosi kufuatana na idadi yao kama walivyokusanywa na Yeieli mwandishi na Maaseya msimamizi chini ya maelekezo ya Hanania, mmojawapo wa maafisa wa mfalme. 12Idadi yote ya viongozi wa jamaa waliowaongoza hawa wapiganaji walikuwa 2,600. 13Chini ya uongozi wao kulikuwa na jeshi la askari 307,500 watu waliofundishwa kwa ajili ya vita, jeshi lenye nguvu la kumsaidia mfalme dhidi ya adui zake. 1426:14 Yer 46:4Uzia akalipatia jeshi lote ngao, mikuki, chapeo, dirii, pinde na mawe ya kombeo. 15Huko Yerusalemu watu wenye utaalamu mkubwa wakatengeneza mitambo iliyotumika katika minara na kwenye pembe za ulinzi ili kurusha mishale na kuvurumisha mawe makubwa. Sifa zake zikaenea mbali sana kwa sababu alisaidiwa mno mpaka akawa na nguvu sana.

1626:16 2Fal 14:10; Kum 32:15; 2Nya 25:19; 1Nya 5:25; 2Fal 16:12-13; Hab 2:4; Kol 2:18; Kum 8:14Lakini baada ya Uzia kuwa na nguvu sana, majivuno yake yakamsababishia kuanguka. Alikosa uaminifu kwa Bwana Mungu wake, naye akaingia hekaluni mwa Bwana ili afukize uvumba kwenye madhabahu ya kufukizia uvumba. 1726:17 1Nya 6:10; 1Fal 4:2; Mdo 26:22Azaria kuhani akiwa pamoja na makuhani wengine themanini wa Bwana wenye ujasiri wakamfuata huko ndani. 1826:18 Hes 16:39; 18:1-7; Kut 30:7; Yer 13:18; 1Nya 6:49; 2Nya 19:2; Mt 14:4; Gal 2:21Wakamkabili na kumwambia, “Siyo sawa kwako, Uzia, kumfukizia Bwana uvumba. Hiyo ni kazi ya makuhani, wazao wa Aroni, ambao wamewekwa wakfu ili kufukiza uvumba. Ondoka mahali patakatifu, kwa kuwa umekosa uaminifu nawe hutaheshimiwa na Bwana.”

1926:19 2Fal 5:25-27; Hes 12:10Uzia, ambaye alikuwa na chetezo mkononi mwake tayari kufukiza uvumba, akakasirika. Alipokuwa anawaghadhibikia makuhani mbele ya madhabahu ya kufukizia uvumba katika Hekalu la Bwana, ukoma ukamtokea penye kipaji chake cha uso. 2026:20 Es 6:12Azaria kuhani mkuu pamoja na makuhani wengine wote walipomtazama wakaona kwamba alikuwa na ukoma penye kipaji chake cha uso wakaharakisha kumtoa nje. Naam, hata yeye mwenyewe alikuwa anatamani kuondoka kwa sababu Bwana alikuwa amempiga.

2126:21 Law 13:46; 14:8; Kut 4:6; 2Fal 15:5; Hes 5:2Mfalme Uzia alikuwa na ukoma mpaka siku ya kufa kwake. Akatengwa katika nyumba ya pekee akiwa mwenye ukoma, naye akawa ametengwa kutoka Hekalu la Bwana. Yothamu mwanawe akawa msimamizi wa jumba la mfalme, pia akawaongoza watu wa nchi.

2226:22 2Fal 15:1; Isa 6:1Matukio mengine ya utawala wa Uzia, kuanzia mwanzo mpaka mwisho, yameandikwa na nabii Isaya mwana wa Amozi. 2326:23 2Fal 15:7; Isa 6:1Uzia akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa karibu nao katika shamba la kuzikia lililokuwa mali ya wafalme, kwa kuwa watu walisema, “Alikuwa na ukoma.” Yothamu mwanawe akawa mfalme baada yake.