1 Wafalme 13 – Kiswahili Contemporary Version NEN

Kiswahili Contemporary Version

1 Wafalme 13:1-34

Mtu Wa Mungu Kutoka Yuda

113:1 Kum 33:1; Amo 7:13Kwa neno la Bwana, mtu wa Mungu alifika Betheli kutoka Yuda wakati Yeroboamu alipokuwa amesimama kando ya madhabahu ili kutoa sadaka. 213:2 2Fal 23:15-16, 20; Law 26:30Akapiga kelele dhidi ya madhabahu kwa neno la Bwana: “Ee madhabahu, madhabahu! Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika nyumba ya Daudi. Juu yako atawatoa dhabihu makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia miungu wale ambao wanatoa sadaka hapa sasa, nayo mifupa ya wanadamu itachomwa juu yako.’ ” 313:3 Mwa 24:14; Yn 2:11Siku iyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo ishara Bwana aliyotangaza: Madhabahu haya yatapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.”

4Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamate!” Lakini mkono aliokuwa ameunyoosha kumwelekea yule mtu ukasinyaa na kubaki hapo hapo, kiasi kwamba hakuweza kuurudisha. 5Pia, madhabahu yalipasuka na majivu yakamwagika sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno la Bwana.

613:6 Mwa 20:7; Mdo 8:24Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwa Bwana Mungu wako ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwa Bwana, nao mkono wa mfalme ukapona na kuwa kama ulivyokuwa hapo kwanza.

713:7 1Sam 9:7Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani kwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”

813:8 Hes 22:18Lakini yule mtu wa Mungu akamjibu mfalme, “Hata kama ungenipa nusu ya mali zako, nisingekwenda pamoja na wewe, wala nisingekula mkate au kunywa maji hapa. 9Kwa kuwa niliagizwa kwa neno la Bwana: ‘Kamwe usile mkate wala usinywe maji au kurudi kwa njia uliyojia.’ ” 10Kwa hiyo akafuata njia nyingine na hakurudi kupitia njia ile ambayo alikuwa ameijia Betheli.

11Basi kulikuwepo na nabii fulani mzee aliyekuwa anaishi Betheli, ambaye wanawe walikuja kumwambia yote ambayo mtu wa Mungu alikuwa ameyafanya pale siku ile. Pia wakamwambia baba yao yale aliyomwambia mfalme. 12Baba yao akawauliza, “Ameelekea njia gani?” Nao wanawe wakamwonyesha ile njia yule mtu wa Mungu kutoka Yuda aliyopita. 13Hivyo akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda.” Walipokwisha kumtandikia punda, akampanda 14na kumfuatilia yule mtu wa Mungu. Akamkuta ameketi chini ya mwaloni na akamuuliza, “Je, wewe ndiwe mtu wa Mungu kutoka Yuda?”

Akamjibu, “Mimi ndiye.”

15Basi nabii akamwambia, “Karibu nyumbani pamoja na mimi ule.”

1613:16 1Fal 13:8Yule mtu wa Mungu akasema, “Siwezi kurudi na kwenda nawe, wala siwezi kula mkate au kunywa maji pamoja nawe mahali hapa. 17Nimeambiwa kwa neno la Bwana: ‘Kamwe usile mkate au kunywa maji huko au kurudia njia uliyojia.’ ”

1813:18 1Fal 22:6; Mwa 19:14Yule nabii mzee akajibu, “Mimi pia ni nabii, kama wewe. Naye malaika alisema nami kwa neno la Bwana: ‘Mrudishe aje katika nyumba yako ili apate kula mkate na kunywa maji.’ ” (Lakini alikuwa akimwambia uongo.) 19Hivyo mtu wa Mungu akarudi pamoja naye na akala na kunywa katika nyumba yake.

20Wakati walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia yule nabii mzee aliyemrudisha huyo mtu wa Mungu. 2113:21 1Sam 13:14Akampazia sauti yule mtu wa Mungu aliyekuwa ametoka Yuda, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Umeasi neno la Bwana na hukushika amri uliyopewa na Bwana Mungu wako, 22bali ulirudi na ukala mkate na kunywa maji mahali ambapo alikuambia usile wala usinywe. Kwa hiyo maiti yako haitazikwa katika kaburi la baba zako.’ ”

23Wakati huyo mtu wa Mungu alipomaliza kula na kunywa, nabii aliyekuwa amemrudisha akamtandikia punda wake. 2413:24 1Fal 20:36Alipokuwa akienda akakutana na simba njiani, akamuua na maiti yake ikabwagwa barabarani, yule punda wake na simba wakiwa wamesimama karibu yake. 25Baadhi ya watu waliopita pale waliona maiti imebwagwa pale chini, simba akiwa amesimama kando ya maiti, wakaenda na kutoa habari katika mji ambao nabii mzee aliishi.

2613:26 1Fal 13:21Yule nabii aliyekuwa amemrudisha kutoka safari yake aliposikia habari hii akasema, “Ni yule mtu wa Mungu ambaye aliasi neno la Bwana. Bwana amemtoa kwa simba, ambaye amemrarua na kumuua, sawasawa na neno la Bwana lilivyokuwa limemwonya.”

27Nabii akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda,” nao wakafanya hivyo. 28Kisha akatoka akaenda akakuta maiti imebwagwa chini barabarani, punda na simba wakiwa wamesimama kando yake. Simba hakuwa amekula ile maiti wala kumrarua punda. 29Basi yule nabii mzee akachukua maiti ya mtu wa Mungu, akailaza juu ya punda na akairudisha katika mji wake, ili amwombolezee na kumzika. 3013:30 Yer 22:18Kisha akailaza ile maiti katika kaburi lake huyo nabii mzee, nao wakaomboleza juu yake na kusema, “Ee ndugu yangu!”

3113:31 2Fal 23:18Baada ya kumzika, akawaambia wanawe, “Wakati nitakapokufa, mnizike kwenye kaburi alimozikwa huyu mtu wa Mungu; lazeni mifupa yangu kando ya mifupa yake. 3213:32 Law 26:30; 1Fal 16:24, 28Kwa maana ujumbe alioutangaza kwa neno la Bwana dhidi ya madhabahu huko Betheli na dhidi ya madhabahu yote katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Samaria, hakika yatatokea kweli.”

33Hata baada ya haya, Yeroboamu hakubadili njia zake mbaya, lakini mara nyingine tena akaweka makuhani kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia miungu kutoka watu wa aina zote. Yeyote aliyetaka kuwa kuhani alimweka wakfu kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia miungu. 3413:34 1Fal 14:10; Yer 35:17Hii ilikuwa ndiyo dhambi ya nyumba ya Yeroboamu ambayo iliisababishia kuanguka na kuangamia kwake hadi kutoweka kwenye uso wa dunia.