Matendo Ya Mitume 4:1-22

Petro Na Yohana Wakamatwa

Walipokuwa bado wanasema na watu, makuhani, mkuu wa walinzi wa Hekalu na Masadukayo waliwajia wakiwa wamekasirika kwa sababu Petro na Yohana walikuwa wakiwafundisha watu kwamba kufu fuka kwa Yesu kunadhihirisha kwamba wafu watafufuka. Wakawaka mata wakawaweka jela mpaka kesho yake kwa maana ilikuwa jioni. Lakini wengi wa wale waliosikia mahubiri yao waliamini; idadi ya wanaume walioamini ilikuwa kama elfu tano.

Siku ya pili yake viongozi wa Kiyahudi, wazee na waandishi wa sheria walikusanyika Yerusalemu. Walikuwepo Kuhani Mkuu Anasi, Kayafa , Yohana, Aleksanda na ndugu zake Kuhani Mkuu. Wakawaleta wale mitume wawili katikati yao wakawauliza, “Ni kwa uwezo gani au mmetumia jina la nani kufanya jambo hili?” Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu akajibu, “Waheshimiwa viongozi na wazee wa watu, kama mnatuhoji kuhusu mambo mema aliyotendewa kilema, na jinsi alivyoponywa, tungependa ninyi na watu wote wa Israeli mfahamu kwamba, ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akam fufua kutoka kwa wafu, kwa uwezo wa Yesu, huyu mtu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa. Huyu Yesu ndiye ‘lile jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa, ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’ Wokovu unapatikana kwake tu; kwa maana hakuna jina jingine duniani ambalo wamepewa wanadamu kuwaokoa ila jina la Yesu, na ni kwa jina hilo peke yake tunaweza kuokolewa!”

Ujasiri Wa Petro Na Yohana Washangaza Watu

Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kufahamu ya kuwa walikuwa watu wa kawaida wasio na elimu walishangaa sana. Wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu. Lakini kwa kuwa walimwona yule kilema aliyeponywa ame simama nao hawakuweza kusema lo lote kupinga maneno yao. Wakawaamuru watoke nje ya ule ukumbi. Kisha wakaanza kuulizana, “Tuwafanye nini watu hawa? Hatuwezi kukanusha muujiza huu mkubwa walioufanya ambao ni dhahiri kwa kila mtu Yerusalemu. Lakini tunaweza kuzuia jambo hili lisiendelee kuenezwa kwa watu kama tukiwakanya wasiseme tena na mtu ye yote kwa jina la Yesu.” Kwa hiyo wakawaita tena ndani wakawaamuru wasiseme au kufundisha watu tena kwa jina la Yesu.

Bora Kumtii Mungu Kuliko Wanadamu

Ndipo Petro na Yohana wakawajibu, “Ninyi amueni wenyewe lililo bora kutenda mbele za Mungu: kuwatii ninyi au kumtii Mungu. Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”

Wale viongozi wakawaonya tena kwa vitisho, kisha waka waacha waende. Hawakuona njia ya kuwaadhibu kwa kuwa waliwaogopa wale watu ambao walishuhudia ule muujiza uliotendeka, nao wali kuwa wakimsifu Mungu. Na yule mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa zaidi ya miaka arobaini.

Read More of Matendo Ya Mitume 4