Esta 2:19-23, Esta 3:1-15, Esta 4:1-17, Esta 5:1-14 NEN

Esta 2:19-23

Mordekai Afunua Hila

2:19 Es 4:2Wakati mabikira walikusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi katika lango la mfalme. Lakini Esta alikuwa ameficha siri ya kabila lake na uraia wake, kama Mordekai alivyokuwa amemwambia, kwa maana aliendelea kufuata maelekezo ya Mordekai kama alivyokuwa akifanya alipokuwa akimlea.

Wakati Mordekai alikuwa ameketi kwenye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, maafisa wawili wa mfalme waliokuwa walinzi wa lango, walikasirika na kupanga njama ya kumuua Mfalme Ahasuero. Lakini Mordekai aligundua hila hii na kumwambia Malkia Esta, ambaye baadaye alimwarifu mfalme, huku akimsifu Mordekai. 2:23 Mwa 40:19; Mhu 10:8Taarifa hiyo ilipochunguzwa na kuonekana kuwa kweli, maafisa hao wawili waliangikwa juu ya miti ya kunyongea. Haya yote yaliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.

Read More of Esta 2

Esta 3:1-15

Hila Ya Hamani Kuwaangamiza Wayahudi

3:1 Hes 24:7; 1Sam 14:48; Hes 24:7; 1Sam 14:48Baada ya matukio haya, Mfalme Ahasuero alimheshimu Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, akampandisha na kumpa kiti chake cha heshima cha juu sana kuliko wakuu wengine wote. 3:2 Dan 3:12Maafisa wote wa mfalme waliokaa langoni mwa mfalme walipiga magoti na kumpa Hamani heshima, kwa kuwa mfalme alikuwa ameamuru hili kuhusu Hamani. Lakini Mordekai hakumpigia magoti wala kumheshimu.

Kisha maafisa wa mfalme waliokuwa langoni mwa mfalme walimuuliza Mordekai, “Kwa nini hutii agizo la mfalme?” 3:4 Mwa 39:10Siku baada ya siku walizungumza naye lakini hakukubali. Kwa hiyo walimweleza Hamani kuona kama tabia ya Mordekai itaweza kuvumiliwa, kwa maana alikuwa amewaambia kuwa yeye ni Myahudi.

Wakati Hamani alipoona kuwa Mordekai hampigii magoti wala kumpa heshima alighadhibika. 3:6 Mit 16:25; Za 74:8Hata hivyo baada ya kujulishwa watu wa Mordekai ni akina nani, alibadili wazo la kumuua Mordekai peke yake. Badala yake Hamani alitafuta njia ya kuwaangamiza watu wote wa Mordekai, yaani, Wayahudi, walio katika ufalme wote wa Ahasuero.

3:7 Es 9:24, 26; 1Sam 10:21Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Mfalme Ahasuero, katika mwezi wa kwanza uitwao Nisani, walipiga puri (yaani kura) mbele ya Hamani ili kuchagua siku na mwezi. Kura ikaangukia kwenye mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari.

3:8 Mdo 16:20-21; Ezr 4:15Kisha Hamani akamwambia Mfalme Ahasuero, “Wako watu fulani wameenea na kutawanyika miongoni mwa watu katika majimbo yote ya ufalme wako, ambao desturi zao ni tofauti na zile za watu wengine wote, nao hawatii sheria za mfalme. Haifai mfalme kuwavumilia watu hawa. Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta 10,0003:9 Talanta 10,000 za fedha ni sawa na tani 340. za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.”

Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kwenye kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui wa Wayahudi. Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.”

3:12 Neh 13:24; Mwa 38:18Kisha siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza waandishi wa mfalme waliitwa. Wakaandika barua kwa kila jimbo na katika kila lugha ya watu kama agizo la Hamani lilivyotoka kwa mfalme, kwa watawala wa majimbo mbalimbali, na wakuu wa watu mbalimbali. Hizi ziliandikwa kwa jina la Mfalme Ahasuero mwenyewe na kutiwa muhuri wa pete yake mwenyewe. 3:13 Es 8:11Barua zilipelekwa na tarishi katika majimbo yote ya mfalme zikiwa na amri ya kuharibu, kuua na kuangamiza Wayahudi wote, wadogo kwa wakubwa, wanawake na watoto wadogo, siku moja, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, na pia kuteka nyara vitu vyao. Nakala ya andiko la amri ilipaswa kutolewa kama sheria katika kila jimbo, na kufahamishwa kwa watu wa kila taifa ili waweze kuwa tayari kwa siku ile.

3:15 Es 8:15Kwa kuharakishwa na amri ya mfalme, matarishi walikwenda na andiko lilitolewa katika mji wa ngome ya Shushani. Mfalme na Hamani waliketi na kunywa, lakini mji wa Shushani ulifadhaika.

Read More of Esta 3

Esta 4:1-17

Mordekai Amshawishi Esta Kusaidia

4:1 Eze 27:30-31; Za 30:11Mordekai alipojua yote yaliyokwisha kufanyika, alirarua mavazi yake na kuvaa nguo za magunia na kujipaka majivu, akaenda mjini, akiomboleza kwa sauti na kwa uchungu. Alikwenda akasimama nje ya lango la mfalme, kwa sababu hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia akiwa amevaa nguo za magunia. Katika kila jimbo ambapo amri na agizo la mfalme lilifika, kulikuwa na maombolezo makuu miongoni mwa Wayahudi pamoja na kufunga, kulia na kuomboleza. Watu wengi wakalala juu ya nguo za magunia na majivu.

Wajakazi wa Esta na matowashi walipokuja na kumwambia kuhusu Mordekai, alipatwa na huzuni kuu. Alimtumia nguo avae badala ya nguo za magunia, lakini Mordekai hakuzikubali. Ndipo Esta akamwita Hathaki, mmojawapo wa matowashi wa mfalme ambaye alikuwa amewekwa kumhudumia Esta, akamwagiza kutafuta ni nini kilikuwa kikimtaabisha Mordekai na ni kwa nini.

Basi Hathaki alitoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanja ulio wazi wa mji mbele ya lango la mfalme. 4:7 Es 7:4Mordekai akamwambia kila kitu ambacho kimempata, pamoja na hesabu kamili ya fedha ambazo Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme kwa ajili ya maangamizi ya Wayahudi. Akampa nakala ya andiko la amri kwa ajili ya maangamizi yao, lililokuwa limechapishwa huko Shushani, kumwonyesha Esta na kumwelezea. Mordekai akamwambia towashi amshawishi Esta kwenda mbele ya mfalme kuomba rehema na kumsihi kwa ajili ya watu wake.

Hathaki akarudi kwa Esta na kumwarifu alilolisema Mordekai. Kisha Esta akamwamuru Hathaki amweleze Mordekai, 4:11 Dan 2:9; Za 125:3“Maafisa wote wa mfalme na watu wa majimbo ya ufalme wanajua kuwa mwanaume au mwanamke yeyote ambaye ataingia kumwona mfalme katika ua wa ndani bila kuitwa, mfalme ana sheria moja tu: Atauawa. Njia pekee kinyume na hili ni mfalme kumnyooshea fimbo ya dhahabu ili aishi. Lakini siku thelathini zimepita tangu nilipoitwa kwenda kwa mfalme.”

Wakati Mordekai aliarifiwa maneno ya Esta, Mordekai alirudisha jibu hili: “Usifikiri kwamba kwa sababu uko katika nyumba ya mfalme wewe pekee katika Wayahudi wote utapona. 4:14 Ay 34:29; Mhu 3:7; Amo 5:13Kwa kuwa kama utakaa kimya wakati huu, msaada na ukombozi kwa Wayahudi utatoka mahali pengine, lakini wewe na jamaa ya baba yako mtaangamia. Nani ajuaye kwamba hukuja kwenye nafasi ya mamlaka kwa ajili ya wakati kama huu?”

Kisha Esta alituma jibu hili kwa Mordekai: 4:16 2Nya 20:3; Mwa 43:14“Nenda, kusanya pamoja Wayahudi wote walioko Shushani, nanyi mfunge kwa ajili yangu. Msile wala kunywa kwa siku tatu, usiku na mchana. Mimi na wajakazi wangu tutafunga kama mnavyofanya. Baada ya kufanyika hili, nitakwenda kwa mfalme, hata ingawa ni kinyume cha sheria. Ikiwa ni kuangamia na niangamie.”

Kwa hiyo Mordekai alikwenda zake na kutekeleza maagizo yote ya Esta.

Read More of Esta 4

Esta 5:1-14

Ombi La Esta Kwa Mfalme

5:1 Eze 16:13; Mit 21:1Siku ya tatu, Esta alivaa mavazi yake ya kimalkia, naye akasimama katika ua wa ndani wa jumba la mfalme, mbele ya ukumbi wa mfalme. Naye mfalme alikuwa akiketi katika kiti chake cha kifalme katika ukumbi, akielekea langoni. Alipomwona Malkia Esta amesimama uani alipendezwa naye, akamnyooshea fimbo ya utawala ya dhahabu ile iliyokuwa mkononi mwake. Kwa hiyo Esta alikaribia na kuigusa ncha ya fimbo ya mfalme.

5:3 Es 7:2; Mk 6:23Kisha mfalme aliuliza, “Malkia Esta, ni nini? Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme, utapewa.”

Esta akajibu, “Kama itampendeza mfalme, mfalme pamoja na Hamani waje leo katika karamu ambayo nimeiandaa kwa ajili yake.”

Mfalme akasema, “Mleteni Hamani mara moja, ili tupate kufanya lile Esta analoomba.”

Kwa hiyo mfalme na Hamani walihudhuria karamu aliyoiandaa Esta. 5:6 Dan 5:16Walipokuwa wakinywa mvinyo mfalme akamuuliza Esta tena, “Sasa haja yako ni nini? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.”

Esta akajibu, “Haja yangu na ombi langu ni hili: 5:8 Es 2:15; 1Fal 3:15Kama mfalme ameona vyema, nami nimepata kibali kwake na kama ikimpendeza mfalme kunipa ombi langu na kunitimizia haja yangu, mfalme na Hamani waje kwangu kesho katika karamu nitakayowaandalia. Kisha nitajibu swali la mfalme.”

Ghadhabu Ya Hamani Dhidi Ya Mordekai

5:9 Mit 14:17Hamani alitoka siku hiyo kwa furaha na moyo mchangamfu. Lakini alipomwona Mordekai langoni mwa mfalme na kuona kwamba hakusimama wala hakuonyesha hofu mbele yake, alijawa na ghadhabu dhidi ya Mordekai. 5:10 Es 6:13Hata hivyo, Hamani alijizuia akaenda zake nyumbani.

Akawaita pamoja rafiki zake na Zereshi, mkewe. 5:11 Mit 13:16; Es 9:10, 13Hamani akajisifia kwao juu ya utajiri wake mwingi, wanawe wengi na kwa njia zote ambazo mfalme amemheshimu kwazo na jinsi alivyomweka juu ya wakuu na maafisa wengine. Hamani akaongeza, “Si hayo tu. Mimi ndiye mtu pekee ambaye Malkia Esta amemwalika kumsindikiza mfalme kwenye karamu aliyomwandalia. Naye amenialika pamoja na mfalme kesho. Lakini haya yote hayanipi kuridhika iwapo ninaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai akiketi kwenye lango la mfalme.”

5:14 Es 7:9; Ezr 6:11Zereshi mkewe na rafiki zake wote wakamwambia, “Tengeneza mahali pa kuangika watu kimo chake dhiraa hamsini,5:14 Dhiraa 50 ni sawa na mita 22.5. kisha kesho asubuhi mwombe mfalme Mordekai aangikwe juu yake. Ndipo uende na mfalme kwenye karamu kwa furaha.” Shauri hili lilimpendeza Hamani, naye akajenga mahali pa kuangika watu.

Read More of Esta 5