1 Wafalme 20:1-43, 1 Wafalme 21:1-29 NEN

1 Wafalme 20:1-43

Ben-Hadadi Aishambulia Samaria

20:1 1Fal 15:18; 13:32Wakati huu, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote. Akifuatana na wafalme thelathini na wawili wakiwa na farasi na magari ya vita, akakwea kuuzingira kwa jeshi Samaria na kuishambulia. Akawatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Fedha yako na dhahabu ni yangu, nao wake zako walio wazuri sana na watoto ni wangu.’ ”

Mfalme wa Israeli akajibu, “Iwe kama usemavyo, bwana wangu mfalme. Mimi na vyote nilivyo navyo ni mali yako.”

Wale wajumbe wakaja tena na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Nimetuma kutaka fedha yako na dhahabu, wake zako na watoto wako. Lakini kesho wakati kama huu, nitawatuma maafisa wangu kukagua jumba lako la kifalme na nyumba za maafisa wako. Watatwaa kitu unachokithamini nao watakichukua.’ ”

20:7 1Sam 11:3; 2Fal 5:7Mfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi na akawaambia, “Tazama jinsi mtu huyu anavyochokoza! Wakati alipotuma apelekewe wake zangu na watoto wangu, fedha zangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.”

Wazee na watu wote wakajibu, “Usimsikilize, wala usiyakubali matakwa yake.”

Kwa hiyo akawajibu wajumbe wa Ben-Hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme, ‘Mtumishi wako atafanya yote uliyoyadai mwanzoni, lakini dai hili la sasa siwezi kulitekeleza.’ ” Wakaondoka na kupeleka jibu kwa Ben-Hadadi.

20:10 2Sam 22:43Kisha Ben-Hadadi akatuma ujumbe mwingine kwa Ahabu, kusema “Miungu iniletee maafa, tena makubwa zaidi, ikiwa vumbi la Samaria litatosheleza konzi moja ya kila mtu ya wale wafuatanao nami.”

20:11 Mit 27:1; Amo 2:14Mfalme wa Israeli akajibu, “Mwambieni, ‘Yule anayevaa mavazi ya vita asije akajisifu kama yule anayevua.’ ”

20:12 1Fal 16:9; 20:13Ben-Hadadi alisikia ujumbe huu wakati ambapo yeye na wafalme walikuwa wanakunywa katika mahema yao, na akawaamuru watu wake, “Jiandaeni kushambulia.” Kwa hiyo wakajiandaa kuushambulia mji.

Ahabu Amshinda Ben-Hadadi

20:13 Amu 6:8; Kut 6:7Wakati ule ule nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Je, unaona jeshi hili kubwa? Nitalitia mkononi mwako leo, nawe ndipo utajua kwamba mimi ndimi Bwana.’ ”

20:14 Amu 1:1Ahabu akauliza, “Ni nani atakayefanya hili?”

Nabii akamjibu, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Maafisa vijana majemadari wa majimbo watafanya hili.’ ”

Akauliza, “Ni nani atakayeanzisha vita?”

Nabii akamjibu, “Ni wewe.”

Kwa hiyo Ahabu akawaita maafisa vijana majemadari wa majimbo, wanaume 232. Kisha akawakusanya Waisraeli wote waliobaki, jumla yao 7,000. 20:16 1Fal 16:9Wakaondoka wakati wa adhuhuri, Ben-Hadadi na wale wafalme thelathini na wawili walioungana naye walipokuwa katika mahema yao wakilewa. Maafisa vijana majemadari wa majimbo waliondoka kwanza.

Wakati huu Ben-Hadadi alikuwa amewatuma wapelelezi, ambao walileta taarifa kusema kwamba, “Askari wanasonga mbele kutoka Samaria.”

Akasema, “Ikiwa wamekuja kwa amani, wakamate wakiwa hai; ikiwa wamekuja kwa vita, wakamate wakiwa hai.”

Wale maafisa vijana majemadari wa majimbo wakatoka nje ya mji jeshi likiwa nyuma yao, kila mmoja akamuua adui yake. Hii ilisababisha Waaramu kukimbia, huku Waisraeli wakiwafuatia. Lakini Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akatoroka akiwa amepanda farasi wake pamoja na baadhi ya wapanda farasi wake. Mfalme wa Israeli akasonga mbele na kushinda farasi na magari ya vita na kusababisha hasara kubwa kwa Waaramu.

20:22 2Sam 11:1Baadaye nabii akaja kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Jiandae vizuri ufikirie la kufanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Aramu atakuja kukushambulia tena.”

Wakati ule ule, maafisa wa mfalme wa Aramu wakamshauri, wakamwambia, “Miungu yao ni miungu ya vilimani. Ndiyo sababu walikuwa na nguvu sana kutuzidi. Lakini kama tukipigana nao katika nchi tambarare, hakika tutawashinda. Fanya hivi: Waondoe hao wafalme wote thelathini na wawili kutoka nafasi zao na uweke maafisa wengine mahali pao. Ni lazima pia uandae jeshi jingine kama lile ulilopoteza, farasi kwa farasi, gari la vita kwa gari la vita, ili tuweze kupigana na Israeli katika nchi tambarare. Kisha kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko wao.” Akakubaliana nao naye akashughulika ipasavyo.

20:26 2Fal 13:17Mwaka uliofuata, majira kama hayo, Ben-Hadadi akawakusanya Waaramu mpaka Afeki kupigana dhidi ya Israeli. 20:27 Amu 6:6; 1Sam 13:6Baada ya Waisraeli kukusanywa na kupewa mahitaji, walikwenda kukabiliana nao. Waisraeli wakapiga kambi mkabala nao kama makundi mawili madogo ya mbuzi, wakati Waaramu walienea katika nchi yote.

20:28 Kut 6:7; Yer 16:19-21Mtu wa Mungu akaja na kumwambia mfalme wa Israeli, “Hivi ndivyo Bwana asemavyo: ‘Kwa sababu Waaramu wanafikiri Bwana ni Mungu wa vilimani na sio Mungu wa mabondeni, nitatia jeshi hili kubwa mkononi mwako, nawe utajua kuwa mimi ndimi Bwana.’ ”

Kwa siku saba walipiga kambi wakitazamana na siku ya saba vita vikaanza. Waisraeli wakawajeruhi askari wa miguu wa Waaramu 100,000 kwa siku moja. 20:30 1Fal 22:25; Za 62:4Waliobaki wakatorokea katika mji wa Afeki, mahali ambapo watu 27,000 waliangukiwa na ukuta. Naye Ben-Hadadi akakimbilia mjini na kujificha kwenye chumba cha ndani.

20:31 Ay 41:3; Mwa 37:34Maafisa wake wakamwambia, “Tazama, tumesikia kwamba wafalme wa nyumba ya Israeli wana huruma. Twendeni kwa mfalme wa Israeli tukiwa tumevaa nguo za gunia viunoni mwetu na kamba kuzunguka vichwa vyetu. Huenda akakuacha hai.”

Wakiwa wamevaa nguo za gunia viunoni mwao na kamba kuzunguka vichwa vyao, walikwenda kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Mtumishi wako Ben-Hadadi anasema: ‘Tafadhali, naomba uniache hai.’ ”

Mfalme akajibu, “Je, bado yuko hai? Yeye ni ndugu yangu.”

Wale watu wakalipokea jambo lile kama dalili nzuri nao wakawa wepesi kulichukua neno lake wakisema, “Ndiyo, yeye ni ndugu yako Ben-Hadadi!”

Mfalme akawaambia, “Nendeni mkamlete.” Ikawa Ben-Hadadi alipokuja, Ahabu akampandisha katika gari lake la vita.

Ben-Hadadi akajitolea, akisema, 20:34 1Fal 15:20; Kut 23:32“Nitairudisha ile miji ambayo baba yangu aliiteka kutoka kwa baba yako. Unaweza kuweka maeneo yako ya soko katika Dameski, kama baba yangu alivyofanya huko Samaria.”

Ahabu akasema, “Katika misingi ya mkataba, nitakuachilia huru.” Kwa hiyo akaweka mkataba naye, akamruhusu aende zake.

Nabii Amlaumu Ahabu

20:35 1Sam 10:5; 1Fal 13:21Kwa neno la Bwana, mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake, “Nipige kwa silaha yako,” lakini yule mtu akakataa.

20:36 1Fal 13:24Kwa hiyo yule nabii akasema, “Kwa sababu hukumtii Bwana, mara tu tutakapoachana utauawa na simba.” Na baada ya yule mtu kuondoka, simba akatokea na kumuua.

Nabii akamkuta mtu mwingine na kumwambia, “Nipige tafadhali.” Kisha yule mtu akampiga na kumjeruhi. Ndipo nabii akaenda na kusimama barabarani akimsubiri mfalme. Akajibadilisha kwa kushusha kitambaa cha kichwani mwake hadi kwenye macho. 20:39 Yos 2:14Mfalme alipopita pale, yule nabii akamwita, “Mtumishi wako alikwenda vitani wakati vita vilipopamba moto, mtu mmoja akanijia na mateka akasema, ‘Mlinde mtu huyu. Kama akitoroka itakuwa uhai wako kwa uhai wake, ama vipande 3,000 vya fedha.’ 20:40 2Sam 12:5Wakati mtumishi wako alipokuwa na shughuli nyingi hapa na pale, yule mtu akatoweka.”

Mfalme wa Israeli akasema, “Hiyo ndiyo hukumu yako. Wewe umeitaja mwenyewe.”

Kisha yule nabii akajifunua macho yake haraka, na mfalme wa Israeli akamtambua kama mmoja wa manabii. 20:42 2Sam 12:7; Yer 48:10Akamwambia mfalme, “Hivi ndivyo Bwana asemavyo: ‘Umemwacha huru mtu niliyekusudia afe. Kwa hiyo ni uhai wako kwa uhai wake, watu wako kwa watu wake.’ ” 20:43 1Fal 21:4Kwa uchungu na hasira, mfalme wa Israeli akaenda kwenye jumba lake la kifalme huko Samaria.

Read More of 1 Wafalme 20

1 Wafalme 21:1-29

Shamba La Mizabibu La Nabothi

21:1 2Fal 9:21; 1Sam 29:1Baada ya hayo, Nabothi, Myezreeli, alikuwa na shamba la mizabibu jirani na jumba la kifalme la Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu nilitumie kwa bustani ya mboga, kwa kuwa liko karibu na jumba langu la kifalme. Badala yake, nitakupa shamba jingine la mizabibu zuri zaidi au, kama utapenda, nitakulipa kiasi chochote unachoona ni thamani yake.”

21:3 Law 25:23Lakini Nabothi akamjibu, “Bwana na apishe mbali kukupa wewe urithi wa baba zangu.”

21:4 1Fal 20:43; Isa 28:23Basi Ahabu akaenda nyumbani, mwenye huzuni na hasira kwa sababu ya yale ambayo Nabothi, Myezreeli, alikuwa amesema, “Sitakupa urithi wa baba zangu.” Akajinyoosha juu ya kitanda akisononeka, na akakataa kula.

Yezebeli mke wake akaingia na akamuuliza, “Kwa nini unahuzunika hivi? Kwa nini huli chakula?”

Akamjibu, “Kwa sababu nilimwambia Nabothi, Myezreeli, ‘Niuzie shamba lako la mizabibu, au kama ukipenda, nitakupa shamba jingine la mizabibu badala yake.’ Lakini akasema, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’ ”

21:7 1Sam 8:14Yezebeli mke wake akasema, “Hivi ndivyo unavyofanya, nawe ni mfalme katika Israeli yote? Inuka na ule! Changamka. Nitakupatia shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli.”

21:8 Mwa 38:18Kwa hiyo akaandika barua kwa jina la Ahabu akaweka muhuri wake juu ya hizo barua, akazipeleka kwa wazee na kwa watu wenye cheo walioishi katika mji pamoja na Nabothi. Katika barua hizo aliandika:

“Tangazeni siku ya watu kufunga na mkamketishe Nabothi mahali pa wazi miongoni mwa watu. 21:10 Kut 22:28; Law 24:15-16; Mdo 6:11Lakini waketisheni watu wawili wabaya kabisa mkabala naye, nao washuhudie kuwa yeye amemlaani Mungu na mfalme. Kisha mtoeni nje na kumpiga kwa mawe hadi afe.”

Hivyo wazee na watu wenye cheo walioishi katika mji wa Nabothi wakafanya kama Yezebeli alivyoelekeza katika barua aliyowaandikia. 21:12 Isa 58:4Wakatangaza mfungo na kumketisha Nabothi mahali pa wazi miongoni mwa watu. 21:13 Law 24:16Kisha watu wawili wabaya kabisa wakaja wakaketi mkabala naye, nao wakaleta mashtaka dhidi ya Nabothi mbele ya watu, wakisema, “Nabothi amemlaani Mungu na mfalme.” Kwa hiyo wakamtoa nje na kumpiga kwa mawe hadi akafa. Kisha wakatuma ujumbe kwa Yezebeli, kusema, “Nabothi amepigwa mawe na amekufa.”

21:15 1Sam 8:14Mara tu Yezebeli aliposikia kwamba Nabothi amepigwa mawe na amekufa, akamwambia Ahabu, “Amka na uchukue lile shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Hayuko hai tena, bali amekufa.” Ahabu aliposikia Nabothi amekufa, akainuka na kushuka ili kulichukua shamba la mizabibu la Nabothi.

Kisha neno la Bwana likamjia Eliya, Mtishbi: “Shuka ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, anayetawala Samaria. Sasa yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ambapo amekwenda alimiliki. 21:19 Ay 24:6; 1Fal 22:38Umwambie, ‘Hivi ndivyo Bwana asemavyo: Je, hujamuua mtu na kuitwaa mali yake?’ Kisha umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Mahali ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba damu yako, naam, yako wewe!’ ”

21:20 1Fal 18:17; Rum 7:14Ahabu akamwambia Eliya, “Kwa hiyo umenipata, wewe adui yangu!”

Akajibu, “Ndiyo, nimekupata. Kwa sababu umejiuza mwenyewe kufanya uovu mbele ya macho ya Bwana. ‘Nitaleta maafa juu yako. Nitaangamiza uzao wako na kukatilia mbali kutoka kwa Ahabu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, wa mtumwa au wa mtu huru. 21:22 1Fal 16:3Nitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwana wa Nebati na ile ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhibisha kwa kuwa umesababisha Israeli kutenda dhambi.’

21:23 2Fal 9:10, 34-36“Pia kwa habari ya Yezebeli Bwana anasema, ‘Mbwa watamla Yezebeli karibu na ukuta wa Yezreeli.’

21:24 1Fal 14:11; Mwa 40:19“Mbwa watawala wale wa nyumba ya Ahabu watakaofia mjini, nao wale watakaofia mashambani wataliwa na ndege wa angani.”

(Hapajapata kamwe kuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza mwenyewe kutenda uovu machoni mwa Bwana, akiwa anachochewa na Yezebeli mkewe. 21:26 Mwa 15:16Alitenda kwa uovu sana katika kuabudu sanamu, kama wale Waamori ambao Bwana aliowafukuza mbele ya Israeli.)

21:27 Mwa 37:34; Yer 4:8; Isa 38:15Ahabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa nguo za gunia na kufunga. Akalala na kujifunika nguo za gunia na kwenda kwa unyenyekevu.

Ndipo neno la Bwana lilipomjia Eliya Mtishbi kusema, 21:29 Kut 32:14; 2Fal 9:26“Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”

Read More of 1 Wafalme 21